Kiukweli maisha halisi ya watanzania wengi tunapotokea maisha yetu ni ya hali ya chini sana ila unafichwa na ule msemo unaosema umaridadi huficha umasikini. Japo nilizaliwa na kukulia Dar kwenye familia ya maisha ya kawaida sana lakini mara tu baada ya kutoka kwenda Iringa niliposoma kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari Malangali hapo ndipo nilipobahatika kuona maisha halisi ya huyu Mtanzania baada ya kuzunguka vijiji mbalimbali katika Mkoa huo wa Iringa.
Nashukuru Mungu nilimaliza masomo yangu na sasa nipo mkoani Tabora kikazi. Kwa miaka 2 tu niliyoishi huku inatosha kujua kwa nini watu wanakimbilia Dar kiukweli maisha ya watu wengi huku ni ya hali ya chini japo mji ni mkongwe na una historia kubwa. Mzunguko wa pesa ni mgumu sana kitu kidogo tu uatazunguka kukipata na ukikipata hiyo bei yake sasa ukiuliza nini utaambiwa gharama za usafirishaji ziko juu. Tumeshazoea kuona mijini majengo ya maana lakini huku unapoingia tu unakutana na nyumba kongwe za tope. Mbaya zaidi mbunge husika yuko Dar yeye kila siku migogoro kwenye klabu kongwe ya mpira wa miguu ya Simba hata siku moja sijawahi kumsikia akielezea matatatizo wa wananchi wake waliompigia kura.
Sikuishia hapo kutokana na kazi yangu nimeweza kutembelea baadhi ya vijiji wilaya mbalimbali za mkoa huu. Huko ndio hakutamaniki maisha yao ni magumu na ya hali ya chini sana lakini kubwa lililonigusa hadi kuandika makala hii ni hishoria ya mtoto mmoja aitwaye Asha Alfred. Mama yake na baba yake wametengana mama yuko mjini na baba ni mfugaji yuko kijijini hivyo mtoto kachukuliwa na baba ambaye ana familia mbili ambazo ziko vijiji tofauti. Mtoto huyu amepelekwa kwa mke mdogo kijiji kingine tofauti na anachoishi huyu baba. kijiji chenyewe kipo mbali na huduma za jamii ni mwendo wa kutosha kutoka nyumba moja hadi kumkuta jirani.
Asha akiwa na familia yake na mama yake mzazi alipomtembelea |
Asha akiwa na familia yake nyuma aliyesimama ni mke mdogo wa baba yake ndiye ambae anaishi na asha kwa sasa |
Maisha ya mtoto huyu ambaye alikuwa tayari ameanza shule ya awali alipokuwa mjini sasa yamekuwa ni ya ufugaji ambayo hayana tena future ya kupata haki yake ya msingi ambayo ni elimu.Na hata kama akiandikishwa bado itakuwa mateso kwake kwani ni umbali mrefu wa kukakiza mapori mpaka kuikuta shule ya msingi ilipo. Lakini haya ndio maisha yetu ya kila siku na wengi wetu tulipotokea japo huwa hatupendi kuzungumzia mara tu tunapopata mafanikio.
Je unafikiri mtu kama huyu anapopata nafasi ya kufika Dar hata kama hatokuwa na pa kulala unadhani atatamani kurudi tena huku kijijini ambako haoni hata future yake?
Picha za Asha akiwa anachunga ng'ombe |
Mdogo wake Asha (Story & photo by Timothy Mwakimbwala) |
No comments:
Post a Comment